Mwandishi Wetu, Inside Tanzania
Tanzania imepongezwa kwa mradi wa ujenzi wa meli mpya ya kisasa ya MV New Mwanza itakayoanza kufanya safari zake katika Ziwa Victoria na kuhudumia nchi za Afrika Mashariki zinazozunguka ziwa hilo.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Waziri wa Maji na Mazingira wa Uganda, Meja Jenerali Mstaafu Kahinda Otafire. Ametoa pongezi hizo wakati wa Mkutano wa 24 wa mawaziri hao uliofanyika jijini Kisumu nchini Kenya Oktoba 23, 2026.
Mkutano huo uliobeba ajenda mbalimbali ikiwemo ya hifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo katika Ziwa Victoria ambapo Otafire ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa mradi huo wa meli ambayo ina uwezo wa usafirishaji wa abiria 1200, mizigo tani 400 za mizigo na magari 20.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa aliyeongoza Ujumbe wa Tanzania amesema fursa hiyo ya mradi wa meli inakwenda kwenye nchi zote ambazo zimepitiwa na ziwa hilo.
Itakumbukwa kuwa ujumbe wa Tanzania chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianao wa Afrika Mashairiki (anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki). Charles Kadonya ulitembelea Bandari ya Kisumu, ili kubadilishana uzoefu, pia kujadili ujio wa Meli ya MV New Mwanza inayotarajia kuanza safari zake hivi karibuni katika Bandari hiyo.
Nchi zinazounda Kamisheni hiyo ni Tanzania, Kenya, Uganda (ambayo ni mwenyekiti kwa sasa), Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na SomaliA.
Katika ziara hiyo, alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha matumizi ya Ziwa Victoria yanakuwa yale yenye kuleta maendeleo endelevu na tija kwa nchi zote wanachama huku tukihakikisha ulinzi wa mazingira.
Katibu Mkuu huyo aliishukuru Serikali ya Kenya kwa ushirikiano inaoutoa katika kuhakikisha Meli ya MV New Mwanza inaanza safari zake katika Bandari ya Kisumu.
“Katika mkutano huu tumesikia Wajumbe kutoka Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamepokewa vizuri mradi huu wa meli na tunahakikisha meli hii inafika nchi zote wanachama ili waweze kusafiri kwa urahisi kutoka eneo moja kwenda lingine, hatua hii ni mafanikio makubwa,” amesema.
Katika hatua nyingine, kupitia mkutano huo umefanyika uzinduzi wa Mpango Mkakati wa namna ya kuendeleza usimamizi wa utunzaji na hifadhi endelevu ya mazingira ya Ziwa Victoria.






Leave a Reply