
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kuratibu mchakato wa kuunganisha mifuko na programu 75 za uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuifanya kuwa mfuko mmoja.
Amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa mitaji na dhamana kwa wananchi, hususan vijana ambao wanakabiliwa na changamoto ya kutimiza masharti ya mikopo katika taasisi za fedha.
Agizo hilo amelitoa wakati wa kukagua maonesho ya vijana kabla ya kushiriki hafla ya kuwasilisha mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha pili, katika sekta ya maendeleo ya vijana. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki, Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ndejembi amesema Serikali imetenga Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana. Amesisitiza kuwa fedha hizo zinapaswa kutolewa kwa haki na bila upendeleo, ili kuwafikia vijana wa mijini na vijijini, wakiwemo vijana wenye ulemavu.
Ameonya kuwa fedha hizo hazipaswi kutumika kulipa posho za watumishi au kununua magari. Badala yake, mafanikio ya mpango huo yapimwe kwa idadi ya biashara zilizoanzishwa, zilizopanuka na ajira zilizozalishwa.
Aidha, amezitaka wizara, taasisi za umma na halmashauri kuhakikisha zinalipa kwa wakati vijana wanaotekeleza zabuni za Serikali ili kuepusha ucheleweshaji wa malipo unaoweza kuathiri shughuli zao za kiuchumi.
Akizungumzia changamoto ya ajira, Ndejembi amesema takribani vijana 900,000 huingia katika soko la ajira kila mwaka, lakini ni takribani mmoja kati ya vijana kumi pekee anayepata ajira rasmi.
Ameeleza kuwa taasisi za umma zimeahidi kutoa takribani nafasi 600 za mafunzo kwa vitendo, ambazo zitatangazwa baada ya taratibu za uratibu kukamilika. Nafasi hizo ni sehemu ya juhudi za kufikia lengo la kutoa nafasi 10,000 katika mashirika ya umma na 20,000 katika sekta binafsi.
Vilevile, amehimiza Mashindano ya AFCON 2027 yatumiwe kama fursa ya kiuchumi kwa vijana. Amesema mafunzo ya muda mfupi yanapaswa kutolewa ili kuwaandaa vijana kutoa huduma mbalimbali kwa wageni watakaohudhuria mashindano hayo.
Ameeleza kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo katika miji ya Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar kutafungua fursa za ajira, kuongeza kipato na kuwawezesha vijana kupata ujuzi utakaowasaidia hata baada ya mashindano kumalizika.
Makamu wa Rais ameipongeza Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kwa juhudi zake za kuwafikia vijana. Pia amewahimiza vijana kutokata tamaa kutokana na changamoto za ajira na mitaji, bali waendelee kujifunza, kubuni na kutumia fursa zinazojitokeza.
Amesema Serikali inaendelea kuandaa mipango mbalimbali kwa ajili ya vijana na kuwataka kuwa tayari kutumia fursa hizo pamoja na kuwasilisha mawazo yao kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Arthur Nanauka, amesema kiasi cha Shilingi bilioni 52.69, sawa na asilimia 26 ya fedha zilizotengwa katika mpango wa Shilingi bilioni 200, kilikuwa kimepelekwa katika wizara zinazohusika na utekelezaji wake.
Amesema mpango huo, kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, umechangia kuzalisha takribani ajira 44,615 kupitia miradi 3,950 katika mwaka wa fedha unaoendelea.
Ameongeza kuwa mikopo inayotolewa kupitia ofisi hiyo haina riba, huku muda wa kuanza kurejesha mikopo ukizingatia mzunguko wa uzalishaji wa shughuli husika.
Akitoa mfano wa wanufaika, Nanauka amemtaja Imani Mpinga, mkulima wa alizeti aliyepata Shilingi milioni 263 kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kusafisha mafuta ya alizeti katika Kijiji cha Makunda. Kiwanda hicho tayari kimeanza kuzalisha na kuuza mafuta.
Kuhusu fursa za manunuzi ya umma, amesema vikundi vya vijana vimepata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 12.99. Serikali inalenga kuongeza thamani hiyo hadi Shilingi bilioni 50 kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha.
Aidha, amesema takribani vijana 400,000 wamejisajili katika mfumo wa Youth Empowerment System (YES), unaowawezesha kupata taarifa kuhusu fursa za ajira na uwezeshaji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Malindi, Muhsin Haji Ussi, akiwasilisha salamu za Umoja wa Wabunge Vijana kwa niaba ya mwenyekiti wake, Zainab Katimba, amesema vijana wanahitaji kuona ahadi zinazotolewa zikitekelezwa na kushirikishwa katika maamuzi yanayohusu maisha na maendeleo yao.
Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa ofisi yenye dhamana mahsusi ya maendeleo ya vijana kumeimarisha uratibu wa masuala ya vijana, ambayo yanahusisha wizara na taasisi mbalimbali.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Dkt. Regina Christopher Malima, akiwasilisha salamu za Bunge, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uratibu wa mipango na bajeti za vijana katika wizara, taasisi za umma na halmashauri.
Amesema Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana inahitaji kupokea taarifa za utekelezaji kutoka sekta mbalimbali ili kufuatilia matumizi ya fedha, maeneo yaliyofikiwa na matokeo yaliyopatikana.
Hafla hiyo imefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Mwaka Mmoja, Vijana Pamoja” na kuhudhuriwa na vijana, viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wabunge, wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, taasisi za fedha pamoja na wadau wa sekta binafsi.





Toa Jibu